JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kufuatia Utabiri wa Hali ya
Hewa uliofanywa kwa pamoja na Mamlaka za Hali ya Hewa kwa nchi za Pembe ya
Afrika na Afrika Mashariki, Mamlaka ya Hali ya Hewa - Tanzania imetoa taarifa
kuhusu uwezekano wa nchi kupata mvua nyingi iliyo juu ya wastani. Hali hii ya
kuwa na mvua nyingi inatabiriwa kuikumba nchi kwa kipindi cha Oktoba, 2012 hadi
Disemba, 2012 na huenda ikaendelea zaidi.
Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa
ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga). Mvua zinatarajiwa kuanza
katika wiki ya tatu ya mwezi Septemba, 2012 katika mkoa wa Kagera na kaskazini
mwa Kigoma na kuendelea kusambaa katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Geita
na Simiyu katika wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2012. Kwa ujumla mvua hizo
zinatarajiwa kuwa juu ya wastani katika maeneo ya Kanda ya Ziwa Viktoria.
Ukanda wa Pwani ya Kaskazini
(Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na Visiwa vya
Unguja na Pemba): Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza ya mwezi wa
Oktoba, 2012. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika
maeneo mengi.
Nyanda za juu Kaskazini
Mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara). Mvua katika maeneo haya
zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili ya mwezi Oktoba, 2012 na zinatarajiwa
kuwa za wastani hadi juu ya wastani.Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma,
Tabora, Katavi na Rukwa).
Mvua zinatarajiwa kuanza katika
wiki ya tatu ya mwezi Oktoba, 2012 katika mkoa wa Kigoma na wiki ya pili ya
mwezi Novemba katika mikoa ya Tabora, Rukwa na Katavi. Mvua zinatarajiwa kuwa
za wastani hadi juu ya wastani katika mikoa ya Rukwa na Kigoma. Aidha maeneo
mengi ya mikoa ya Katavi na Tabora mvua zinatarajiwa kuwa juu ya wastani. Kanda
ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma). Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya
nne ya mwezi Novemba na zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani.
Nyanda za juu Kusini Magharibi
(Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro): Mvua zinatarajiwa
kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Novemba 2012 na zinatarajiwa kuwa za wastani
hadi juu ya wastani katika mkoa wa Njombe na kusini mwa mikoa ya Mbeya na
Morogoro. Maeneo ya kaskazini mwa mikoa ya Mbeya na Iringa, mvua zinatarajiwa
kuwa juu ya wastani. Maeneo ya Kusini na Pwani ya Kusini (mikoa ya Ruvuma, Lindi
na Mtwara): Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Novemba, 2012 na
zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi.
Kwa kuzingatia hali hii Ofisi
ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa tayari imetoa taarifa/elimu
kwa umma kupitia kipindi cha “Tuambie” cha TBC 1 na kuelekeza taasisi na wadau
mbalimbali kuchukua hatua za tahadhari. Mfumo wetu wa kukabiliana na maafa una
Kamati za Maafa kwenye ngazi ya mkoa, wilaya hadi kijiji ambazo zina majukumu
ya kusimamia masuala ya maafa katika maeneo yao. Kamati zilizoanishwa hapo juu
pamoja na wadau wote mnakumbushwa kujiandaa kukabiliana na maafa endapo
yatatokea. Katika jitihada za kujiandaa mnakumbushwa kuzingatia yafuatayo:-
1. Kutekeleza mipango mbadala
katika maeneo mliyobaini kuwa yana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na mafuriko;
kama vile kuhamisha wananchi maeneo ya mabonde kwenda sehemu salama na
kurejesha mawasiliano endapo yataharibika.
2. Kupatikana dawa muhimu za
magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na madawa ya kusafisha maji ya kunywa
(Water Guard Tablets).
3. Kupatikana kwa dawa muhimu
za mifugo kwani magonjwa miguu na midomo (FMD) na homa ya bonde la ufa (RVF) yana
uwezekano mkubwa wa kutokea.
4. Upatikanaji wa chakula cha
kutosha. Aidha wananchi wahimizwe kuweka akiba ya chakula cha kutosha.
5. Kutenga fedha za kukabiliana
na maafa endapo yatatokea.
6. Elimu kwa Umma itolewe kwa
kuhusisha vyombo vyote vya mawasiliano na uongozi wa Vijiji na Mitaa.
7. Kuchukua hatua za ziada kwa
maeneo ambayo yana uwezekano mkubwa wa kuathiriwa na mmomonyoko wa ardhi.
8. Kuainisha mitaro inayoweza
kuingiza maji katika migodi ya wachimbaji wadogowadogo, na kuchukua tahadhari
zinazostahili.
9. Kuhakikisha kuwa mifereji na
mitaro ya maji machafu kwa maeneo ya Jiji/miji iko safi na wazi wakati wote
kupitisha maji.
10. Kuchimba au kukamilisha
uchimbaji wa mabwawa ya kuvuna maji ya mvua.
11. Maofisa Ugani - Kilimo
kutoa ushauri kwa wakati kuhusu mazao ya kupanda na pia wafugaji kutumia nafasi
kuvuna malisho ya kutosha yatakayotumika kipindi cha kiangazi .
12. Kila ngazi kujiweka tayari
kukabiliana na mafuriko ni muhimu kuunda timu za wataalam wa kukabiliana na
athari zitakazotokea, majina yao yaainishwe na waelekezwe cha kufanya pindi
hali ikiwa hivyo.
Ni matumaini yangu kuwa
tukishirikiana katika kukabiliana na mvua nyingi pamoja na majanga
yanayoambatana na mvua hizi, tunayo nafasi kubwa ya kujihakikishia usalama wa
nchi yetu kutokana na majanga ya asili.
Nashukuru kwa ushirikiano wenu.
IMETOLEWA
NA
KATIBU
MKUU, OFISI YA WAZIRI MKUU
No comments:
Post a Comment