Chuo cha Biashara (CBE) tawi la Dodoma, Jumatano ya septemba 12, 2012 kimefanya semina ya kuwatambulisha wanafunzi wapya wa Stashahada na Cheti waliodahiliwa kuanza masomo yao chuoni hapo ili kuweza kujua taratibu na kanuni zinazoendesha chuo hicho.
Kikao hicho kilichohudhuriwa na mlezi wa Wanafunzi wa Chuo hicho tawi la Dodoma Bw. Sikato pamoja na baadhi ya Viongozi wa Serikali ya wanafunzi ya Chuo hicho tawi la Dodoma (COBESO-Dodoma) kilikuwa na lengo la kufahamu mambo mbalimbali katika nyanja za kitaaluma, kijamii na Mazingira ya Chuo hicho katika tawi la Dodoma.
Akianza kwa kuwapongeza wanafunzi hao kwa kuchaguliwa kujiunga na Chuo hicho, Mlezi wa wanafunzi alisema kwamba CBE ni chuo kikongwe kinachotoa elimu bora na kukidhi haja ya wanafunzi hivyo CBE kinatambua na kuthamini kwa dhati uwepo wa wanafunzi hao chuoni hapo.
“Chuo kinatambua na kuthamini uwepo wenu, lakini pia tunawataka nyinyi wenyewe kuthamini uwepo wenu hapa kwani wazazi/walezi wenu wanalipa gharama kubwa ili kuhakikisha mnasoma katika mazingira na hali nzuri ili baadae kwenda kuikomboa jamii yenu inayowazunguka, hivyo ni lazima kuwa makini kwa kile ulichokifuata”. Alisema Bw. Sikato.
Katika mazungumzo yake Mshauri wa wanafunzi alisisitiza na kuzungumzia zaidi juu ya Suala zima la kutii Kanuni na Sheria za Chuo kwa kipindi chote watakachokuwepo chuoni hapo. “Kanuni hizi ziko kwa ajili ya kukulinda wewe ili uweze kusoma vizuri katika mazingira rafiki" alisema mlezi wa wanafunzi.
Bw. Sikato aliongeza kwa kuzungumzia Suala zima la mavazi ambapo alibainisha kwa kusema jambo hili sio geni masikioni mwa wanafunzi hivyo ni vyema kila mmoja akaheshimu na kutii taratibu za mavazi yanayoendana na kulinda heshima na utu wa Mtanzania. “Tumepitisha kanuni na taratibu juu ya swala zima la mavazi hapa chuo, hii inatokana na kuporomoka kwa maadili kwa baadhi ya vijana wetu ambao bila ya aibu wanavaa nguo ambazo huwezi kujua kama wanatoka au ndio wanaenda disko” alisema mlezi huyo.
Akizungumzia suala la siasa vyuoni mlezi wa wanafunzi amekemea vikali na kuwaonya wanafunzi hao kutojihusisha na Masuala ya kisiasa wakiwa katika mazingira ya Chuo na kuwaeleza kuwa chama chao ni COBESO na si vinginevyo. Suala la Mwanafunzi kuwa CCM, CHADEMA, CUF, ADC, TLP n.k ni suala la mtu binafsi na ni vyema itikadi hizo zikafanyika nje ya chuo na kuonya vikali kwa mwanafunzi atakayeonekana kueneza itikadi za kisiasa hapa chuoni.
Akizungumzia suala la Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, Bw. Sikato aliongeza kwa kusema ni vyema wanafunzi wakadumu kwa kuheshimu maadili ya kidini na kuachana na tabia ya uzinzi ili kuepukana na maambukizi hayo "Suala la Maambukizi ya UKIMWI ni janga kubwa barani Afrika na duniani kote, hivyo ni vema tukakumbushana wakati wote tunapokutana kama ilivyo sasa" ingawa kwa wale wanaoshindwa kujizuia ni vema wakajiepusha na ngono zembe kwa kutumia kinga (kondomu) kujikinga na maambukizi hayo.
Kikao hicho kilichohudhuriwa na wanafunzi takribani mia nne, uongozi wa COBESO uliweza kuwatambulisha viongozi waliokuwepo wakati huo na kuwambia ya kuwa ofisi ya COBESO ipo kwa ajili ya kuwasikiliza na kutatua kero na shida zao hivyo wanatakiwa wasiogope kufika ofisini kuomba msaada au kueleza shida zao.
“Tumechaguliwa ili kuweza kuwatumikia nyinyi na kutatua shida zenu zitakazo wakabili chuoni hapa hivyo kila mwanafunzi wa CBE ana uhalali wa kupewa huduma na kusaidiwa katika shida lakini pia kupewa ushauri ili uweze kuishi kwa amani na kutimiza malengo yako” Alisema Kaimu Waziri Mkuu ambae ni Waziri wa Mwasiliano na Mahusiano Bw. Remidius M. Emmanuel.
Kaimu Waziri Mkuu wa COBESO Bw. Remidius M. Emmanuel ambae ni Waziri wa Mawasiliano na Mahusiano akisisitizia jambo kwa wanafunzi wenzake (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha Mlezi wa wanafunzi. |
No comments:
Post a Comment