Sunday, September 16, 2012

KUTOKA CBE-DODOMA: MAKAMU MKUU WA CHUO AKUTANA NA WANAFUNZI WAPYA JUZI IJUMAA, SWALA LA ONGEZEKO LA ADA YA HOSTELI LAIBULIWA.


Makamu mkuu wa Chuo cha Elimu wa Biashara tawi la Dodoma (CBE-Dodoma) Bw.  Omar M. Kiputiputi, juzi Ijumaa amekutana na wanafunzi wapya wanaoingia mwaka wa kwanza kuanza masomo ya Stashada na Cheti katika ukumbi wa mikutano Chuoni hapo katika muendelezo wa Chuo hicho kuwakaribisha mwaka wa kwanza, Ikiwa ni siku chache tu toka wanafunzi hao wapya kukutana na mlezi wa wanafunzi na uongozi wa serikali ya wanafunzi (COBESO-Dodoma).

Akifungua kikao hicho Mkuu huyo wa chuo alianza kwa kuwaambia wanafunzi hao kwamba CBE ni miongoni mwa vyuo vichache vyenye historia ya kipekee nchini Tanzania. “Chuo hiki kilianzishwa mwaka 1965 ambapo wakati kinaanza kilikuwa kinatoa kozi moja tu ya Utawala wa Biashara na kimetoa viongozi na wanataaluma wengi hapa nchini wakiwamo baadhi ya mawaziri na Maprofesa wametokea hapa na mpaka sasa chuo kina jumla ya wanafunzi 3500, licha ya chuo chetu kuwa na changamoto za hapa na pale lakini bado ni hazina” Alisema makamu mkuu wa chuo.

Makamu Mkuu amesema kwamba, Matarajio ya Mzazi/Mlezi/Mfadhili ni kuhakikisha mtoto wake anasoma katika taasisi nzuri itakayompatia elimu bora. Ni jukumu la Mwanafunzi kusoma kwa bidii ili kuweza kufikia malengo hayo baada ya mzazi kutimiza jukumu lake.

“Ni lazima mwanafunzi asome kwa bidii na kwa nguvu zake zote, swala la msingi ni kuzingatia kile ulichokifuata na kuacha ushabiki wa kufata makundi mabaya na sisi kama chuo tutafanya majukumu yetu ya kutafuta walimu bora, vifaa vya ufundishia pamoja na majengo na huduma bora unayotakiwa uipate pindi uwapo chuoni. Hivyo ni heri kabisa uepuke misuguano na kujiingiza katika matatizo pindi uwapo chuoni na uwe na nidhamu kwa jamii inayokuzunguka na kutii sheria zilizowekwa na mamlaka ya chuo” Alisema makamu mkuu wa Chuo.

Akizungumzia Serikali ya wanafunzi (COBESO-Dodoma), Makamu Mkuu wa chuo ameitaja serikali ya wanafunzi kama Daraja baina ya mwanafunzi na Uongozi wa Chuo ambapo mtu anapopatwa na tatizo lolote kuna taratibu anatakiwa afuate na moja ya eneo zuri la kuanzia ni katika serikali ya wanafunzi na wao watalifikisha katika uongozi wa chuo.

Siasa Chuoni

Akigusia swala zima la kufanya siasa chuoni hapo, Makamu Mkuu wa Chuo alitoa onyo kali kwa wanafunzi hao la kutojihusisha na siasa wawapo chuoni hapo kwani chuo hicho si cha kufanyia siasa. “Ninafahamu kuwa wapo wenye itikadi za kisiasa lakini hapa si uwanja wake, atakaebainika kujihusisha na swala zima la siasa chuoni hapa basi sheria za chuo zitachukua mkondo wake kwani hapa si uwanja wa siasa bali ni uwanja wa kitaaluma hivyo ni haturuhusu mtu yoyote kufanya siasa” Alisema Mkuu wa Chuo.

Kupanda kwa ada za Hostel

Suala hili liliibuliwa na mmoja wa wanafunzi Bw. Vicent John Kinene aliyetaka kujua mabadiliko ya ongezeko la ada ya Hosteli za Chuo. “Tumepokea muongozo wa kujiunga na chuo na unaonyesha ada ya hosteli ni 300,000/= kiasi ambacho wazazi wanakitambua, wakati kiwango hicho ni tofauti na cha sasa cha 450,000/= ambapo imeleta mkanganyiko mkubwa kwani hata katika tovuti ya chuo maelezo haya hayapo, Je vigezo gani chuo vimetumia kupandisha ada hiyo?” Aliuliza Bw. Vicent.

Akijibu suala hilo kwa niaba ya makamu mkuu wa chuo, Mshauri wa wanafunzi Bw. Sikato alisema kwamba hatua hiyo ya ongezeko imefikiwa baada ya makubaliano ya kikao cha Bodi ya Chuo ambacho kiliongeza ada ya hosteli na kufikia kiwango hicho, na kuongeza kuwa ada hiyo ni kwa matawi yote ya Dar es salaam, Dodoma na Mwanza na taarifa hizi kwa sasa zimeshawekwa kwenye tovuti ya chuo.

Rais wa wanafunzi Bw. Robert Mwitango nae alipata fursa ya kuliongelea swala hili juu ya hatua ambazo COBESO imeshazichukua na inaendelea kuzichukua. “ Mimi kama rais kwa kusaidiana na viongozi wenzangu, tayari tumeshachukua hatua juu ya swala la ongezeko la ada, nimefanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo pamoja na Waziri wa Biashara na Viwanda Dr. Abdallah Kigoda na bado mazungumzo yanaendelea, imani yangu tutafikia muafaka mzuri hivyo nawaomba tuwe na subira” Alisema Rais huyo wa COBESO.

Akihitimisha hotuba yake Makamu Mkuu wa chuo alisem kwamba kwa kawaida ili chuo kiweze kujiendesha siku zote kinategemea ada za wanafunzi hivyo ni vyema kila mwanafunzi akalipa ada hiyo mapema ili kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza, kwani ni jukumu la kila mwanafuzi kulipa Ada.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) tawi la Dodoma Bw. Omari M. Kiputiputi akitoa hotuba kwa wanafunzi takribani 500 waliohudhuria katika mkutano huo, wanafunzi hao (hawapo pichani) ni wa mwaka wa kwanza ambao ndio wanaanza elimu yao katika ngazi ya Stashahada na Cheti.
Badhi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa ngazi za Cheti na Stashahada wakisikiliza kwa makini hotuba kutoka kwa makamu mkuu wa chuo ndani ya ukumbi wa mikutano chuoni hapo siku ya ijumaa.
Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza ngazi ya stashahada Bw. Vicent John akiuliza swali juu ya swala zima la Ongezeko la ada
Rais wa serikali ya wanafunzi katika Chuo cha Elimu ya Biashara tawi la Dodoma (COBESO-Dodoma) Bw. Robert Mwitango akiongea jambo katika mkutano huo.
 

No comments:

Post a Comment