Hali hiyo inatokana na vyuo hivyo
kuanza kufunguliwa mwishoni mwa mwezi huu na mwanzoni mwa mwezi ujao. Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa
wanafunzi katika vyuo hivyo walioomba mikopo toka HESLB, bado hawajaanza kupata
hatua ambayo imeanza kuwapa shaka kama wataripoti vyuoni kwa wakati kutokana na
kutegemea fedha za mikopo kwa ajili ya ada ya masomo na mahitaji mengine.
Kutokana na ucheleweshaji wa
mikopo hiyo, gazeti hili lilishudia wanafunzi kadhaa ambao wamedahiliwa
kujiunga vyuo vya elimu ya juu mwaka huu, wakimiminika katika ofisi za HESLB
makao makuu jijini Dar es Salaam kuulizia hatma ya mikopo waliyoomba.
“Unavyoniona hapa ni wiki ya tatu
nimekuwa nikija hapa ofisi za Bodi ya Mikopo kuulizia kama mikopo imeanza
kutolewa, lakini tunaelezwa tuendelee kusubiri wakati vyuo vimekaribia
kufunguliwa,” alisema mwanafunzi mmoja aliyetoka Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani
Morogoro.
Hata hivyo, Afisa mmoja wa HESLB,
aliyejitambulisha kwa jina moja la Venelanda, alisema mchakato wa kuandaa
mikopo ya wanafunzi bado unaendelea na kwamba zoezi hilo linachukua muda kidogo
kutokana na mikopo hadi kukamilika kwake hupitia maeneo mengi.
Venelanda ambaye hata hivyo,
hakutoa jibu la moja kwa moja kama mikopo kwa wanafunzi hao itaanza kutolewa
lini, alisema HESLB itahakikisha mikopo hiyo inatolewa kwa wanafunzi hao kabla
ya kufunguliwa vyuo hivyo.
Mkuu wa Idara ya Habari Wizara ya
Fedha, Ingiahedi Mduma, alipoulizwa na gazeti hili kama fedha za mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu zimeshapelekwa
HESLB, alisema suala hilo waulizwe Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
“Bajeti ikishapitishwa bungeni,
kinachobakia ni kwa wizara husika kushughulikia mipango yake, hivyo hata suala
la fedha za mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu
wenye majibu ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,” alisema Mduma.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, Phillipo Mulugo, alipoulizwa na NIPASHE, alisema kimsingi mikopo
bado haijaanza kutolewa kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na kufafanua
kuwa kuanzia wiki hii wizara yake itaangalia uwezekano wa kushughulikia suala
hilo ili wahusika wapewe mikopo hiyo.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Bhokombe Itembe, alisema wanafunzi wa
mwaka wa kwanza wanatarajia kuripoti chuoni hapo Oktoba Mosi, mwaka huu.
Alisema wiki iliyopita uongozi wa
chuo na Daruso, walitaka kupanga vyumba katika hosteli kwa ajili ya wanafunzi,
lakini zoezi hilo lilishindikana kwa sababu bado haijafahamika idadi ya
wanafunzi wa mwaka wa kwanza watakaoripoti chuoni hapo.
Itembe alisema tatizo la
kuchelewa kwa mikopo linatokana na sababu kadhaa, ikiwemo kutokuwepo kwa
ushirikiano kati ya HESLB na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU). “Mwanafunzi
anapodahiliwa bila TCU kumuamulia ataenda chuo gani, huwezi kwenda na wakati
huo huo bila HESLB kukupatia mkopo, vile vile huwezi kwenda chuoni,” alisema
Itembe.
Rais wa Chuo Kikuu cha Usimamizi
wa Fedha IFM, Michael Chazy, alisema chuo hicho kitafunguliwa Oktoba 8, mwaka
huu na kwamba hadi sasa bado wanafunzi wanaoendelea na wale wa mwaka wa kwanza
hawajaanza kupatiwa mikopo.
Naye Rais wa Chuo Kikuu cha
Dodoma (Udom), Paul Yunge, alisema suala la mikopo katika chuo lina utata hasa
kwa wanafunzi wanaoanza mwaka wa kwanza ambapo baadhi yao wamejaza fomu vibaya
na hivyo taasisi husika zinashughulikia tatizo hilo.
Rais wa Chuo Kikuu cha Mzumbe,
Amos Chakushemeire, alisema utoaji wa mikopo hauridhishi kabisa katika chuo
hicho ambapo wanafunzi walioanza muhula Julai, mwaka huu, wamelipwa robo ya
mkopo wakati kiasi kingine cha mkopo hawajalipwa hadi sasa, hali ambayo imesababisha
ukata mkubwa kwa wanafunzi.
“Chuo chetu ni tofauti na
vingine, kina mihula mitatu, wanafunzi walioanza muhula wa Julai hawajalipwa
sehemu nyingine,. Hivi karibuni uongozi wa chuo ulilazimika kuwakopesha Sh.
50,000 wanachuo hao ili kuwatuliza wasigome,” alisema Chakushemeire.
Rais wa Chuo cha Ustawi wa Jamii,
Frank Nkinda, alisema mikopo ni changamoto kubwa katika chuo hicho ambapo
wanafunzi wa mwaka wa kwanza hawajapata mikopo hadi sasa. Alisema kutokana na
hali hiyo, hivi karibu Mwenyekiti wa HESLB alifika chuoni hapo kuzungumza na
uongozi, serikali ya wanafunzi na wanachuo ambapo alitoa ahadi kutoa mikopo kwa
wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika mwaka huu wa 2012/2013.
Mwaka jana serikali kupitia
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilitangaza utaratibu mpya wa utoaji wa
mikopo ambapo badala ya fedha hizo kutolewa kwa waombaji na HESLB, sasa fedha
hizo zinapelekwa vyuoni ambako menejimenti za vyuo zinawajibika kuzisimamia na
kuwapa waombaji. Hatua hiyo ilifikiwa ili kurahisisha mchakato wa kuwapatia
fedha waombaji na pia kuepusha usumbufu kwa HESLB kutokana na wanafunzi kutoka
vyuoni kuvamia ofisi hizo kwa lengo la kushinikiza wapewe fedha.
Taarifa iliyotolewa na HESLB na
TCU Agosti 10 na 12, mwaka huu ilieleza kuwa zaidi ya wanafunzi 3,074 walioomba
mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2012/13, wameenguliwa katika maombi yao
kutokana na dosari mbalimbali. Taarifa hiyo ilieleza kuwa HESLB pekee
iliorodhesha zaidi ya wanafunzi 2,649 ambao ilibaini kuwa na mapungufu kadhaa
katika maombi yao ya kupewa mikopo.
Miongoni mwa makosa ama dosari
ambazo HESLB ilizibaini kwa walioenguliwa ni pamoja na kukosekana kwa vyeti vya
kuzaliwa kwa muombaji, sahihi ya mdhamini/muombaji, kukosekana kwa picha ndogo
ya muombaji/mdhamini, kukosekana kwa sahihi za viongozi wa serikali za
mitaa/vijiji kwa waombaji na nyaraka nyingine muhimu kwa waombaji.
Kwa upande wake TCU, iliwaengua
jumla ya waombaji 425 kwa dosari na makosa mbalimbali. Miongoni mwa dosari ambazo
zilitajwa na TCU ni pamoja na baadhi yao kukosea namba za vyeti vya masomo kwa
vidato vya nne na tano, miaka ya kumaliza masomo, mawasiliano sahihi kwa
muombaji pamoja na uchaguzi wa masomo.
Hata hivyo, taasisi hizo mbili
zimetoa muda kwa walioenguliwa sasa kutokana na dosari hizo kurekebisha na
kutuma tena maombi yao kupitia mitandao kwa mujibu wa maelekezo waliyotoa. Kwa
mwaka huu wa fedha 2012/13, serikali imeiongezea fedha HESLB kwa kuitengea Sh.
bilioni 326 kwa wanafunzi 98,772.
Mwaka jana, serikali iliitengea
HESLB Sh. 91,722,783,264 kwa ajili ya
mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Ucheleweshaji wa fedha za mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu umekuwa ukisababisha wafanye migomo, vurugu na
maandamano mara kwa mara kushinikiza walipwe.
Chanzo Nipashe
No comments:
Post a Comment